Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita, amesema kukamilika kwa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga (Ibadakuli) kutakuwa hatua kubwa ya mageuzi katika sekta za uchumi, biashara, utalii na usafiri wa anga ndani ya mkoa na kwa taifa kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Uwanja huo, Mhe. Mhita alisema:
“Uwekezaji huu mkubwa unaotarajiwa kukamilika hivi karibuni, utafungua milango kwa wafanyabiashara, wakulima na wawekezaji. Tumeuweka uwanja huu kwenye mpango wa kimkakati wa maendeleo ya mkoa ili kuunganisha fursa zilizopo na masoko mapya, ndani na nje ya nchi."

Alisisitiza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kuimarisha mazingira rafiki kwa uwekezaji, hasa kwa kuzingatia uwepo wa Kongani ya Kitaifa ya Biashara ya Buzwagi, ambayo inalenga kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Kiwanja cha Ndege Shinyanga, Lugano Mwinuka, alieleza kuwa mradi umefikia asilimia 90 ya utekelezaji, na kazi kubwa zinazoendelea ni maboresho ya miundombinu ya kiufundi na kiusalama.

“Tunafanya ukarabati wa njia ya kurukia na kutua ndege (runway), maegesho ya ndege, jengo la abiria, mitaro ya maji, taa za usiku, uzio wa usalama na kituo cha hali ya hewa,” alisema.
Aliongeza kuwa kukamilika kwa uwanja huo kutawezesha ndege aina ya Bombardier Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 74 kutua kwa urahisi. Hii ni hatua itakayopandisha hadhi ya kiwanja kutoka daraja la kwanza hadi la tano katika viwango vya zimamoto na usalama wa anga.
Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Chiando Mwinuka, alithibitisha kuwa barabara kuu zote zinazounganisha uwanja huo na mikoa jirani kama Tabora na Mwanza tayari zimekamilika.

“Tumejenga barabara ya kisasa inayoingia moja kwa moja uwanjani. Lengo ni kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, na kuongeza ufanisi wa huduma za anga katika mkoa wetu,” alisema.
Kwa upande wa wananchi, matumaini ni makubwa. Bi. Esther Maziku, mkazi wa Ngokolo, alisema:
“Zamani tulikuwa tukisafiri hadi Mwanza ili tupate ndege tena kwa kutumia muda mrefu lakini Sasa Uwanja tunao wenyewe, tunamshukuru Rais Samia kwa kutenga fedha na kutuletea Uwanja wa Ndege na sasa tunaona kama tumeunganishwa na dunia. Hii ni fursa kwa wanawake wajasiriamali kama mimi.”
Mradi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga unatazamwa kama kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi, hasa kwa kuzingatia utajiri wa rasilimali zilizopo mkoani hapa kuanzia ardhi yenye rutuba, madini, hadi vivutio vya utalii na uwekezaji.
Mradi huo unakadiriwa kugharimu TSh bilioni 52 (pamoja na VAT), ambapo 80% ya fedha zimetolewa na Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya (European Investment Bank) na 20% inagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Kwa kukamilika kwake, uwanja huu utaifanya Shinyanga kuwa kitovu kipya cha biashara na utalii katika Kanda ya Kaskazini Magharibi ya Tanzania, huku ukifungua milango kwa mashirika ya ndege ya ndani na ya kimataifa.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa