Na Johnson James, Shinyanga
Viongozi wa dini mkoani Shinyanga wametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, wakisisitiza kuwa ni haki ya kikatiba na hatua muhimu ya kuchagua viongozi bora watakaowaletea maendeleo ya kweli kuanzia ngazi ya jamii.

Wakizungumza leo Octoba 18, 2025 mkoani Shinyanga kwa pamoja katika tamko lao kwa umma, viongozi hao wakiongozwa na Askofu Dkt Emmanuel Makala wameazimia kuunga mkono jitihada za serikali katika kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi huo kwa amani na utulivu, huku wakikumbusha kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda amani ya nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amewatoa hofu wananchi akiwahakikishia kuwa siku ya uchaguzi itakuwa salama na yenye utulivu, huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiwa tayari kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.
"Tunawahakikishia wananchi usalama wao. Waende kupiga kura bila hofu. Serikali imejipanga kuhakikisha kila mmoja anatekeleza haki yake kwa uhuru,” alisema Mhita.
"Amani ni tunu ya taifa letu. Bila amani hakuna maendeleo. Tunawasihi wananchi kujitokeza kupiga kura kwa utulivu, wakitambua kuwa wanatimiza wajibu wao kwa taifa" walisema viongozi hao kwa umoja wao.

Aidha, aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu ameendelea kuwasihi viongozi wa dini, machifu, na wazee kuendelea kuliombea taifa, hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi, akisisitiza kuwa maombi ni silaha ya kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
Tamko hilo ni sehemu ya juhudi za pamoja za kuhakikisha uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani unafanyika katika hali ya utulivu, mshikamano na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa