Mhadhiri wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo
Dkt. Henry Jonathan akitoa ufafanuzi wa Kiongozi
cha Mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya
wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za
Mitaa kwa Wakuu wa Sehemu na Vitengo katika
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga tarehe 16/08/2017.
Waajiri nchini wametakiwa kutoa mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya katika Sekta za Umma ili kuwapa watumishi hao taarifa sahihi kuhusu haki na wajibu wao wakiwa kazini.
Akitoa ufafanuzi wa kijitabu cha mwongozo wa utaratibu wa mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kikao cha pamoja na Wakuu wa Sehemu na Vitengo wa Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga, mapema wiki hii, mmoja wa washiriki katika kuandaa mwongozo huo, Dkt. Henry Jonathan amesema changamoto nyingi wanazokumbana nazo waajiriwa wapya zinatokana na kukosa taarifa sahihi hivyo kupelekea kukata tamaa na kupoteza morali ya kazi.
Dkt. Henry ambaye ni Mhadhiri wa Chuo cha Serikali za Mitaa – Hombolo Dodoma amesema kuwa, baadhi ya waajiri hawatoi mafunzo kwa waajiriwa wapya kutokana na kutojua umuhimu wa mafunzo hayo pamoja na uhaba wa fedha.
Amesema wakati mwingine mafunzo hayatolewi kwa wakati hivyo kupelekea watumishi hao kufanya vitu ambavyo si sahihi.
Kijitabu hicho ambacho kilishazinduliwa na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. George Simbachawene kinaeleza utaratibu mzima wa namna ya kuwapokea watumishi wapya katika ajira na kuwapa mafunzo elekezi ili kuendana na Sera, Sheria na taratibu za kiutumishi kuanzia ngazi ya Wizara hadi vijiji.
Kijitabu hicho kilichotengenezwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta ya Umma (PS3) kitasambazwa katika Mikoa yote nchini ili kiwasaidie waajiri kutoa mafunzo elekezi kwa watumishi wapya katika ajira.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa