Serikali Mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na Viongozi wa dini wameazimia kwa pamoja kuwatambulisha waandikishaji wa wanachama wa mfuko wa Afya wa Bima ya Wananchi yaani CHF kwenye nyumba za Ibada ili kupanua wigo wa uandikishaji wa mfuko huo.
Azimio hilo limefikiwa katika kikao cha pamoja kati ya Mkoa na viongozi hao wa dini kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kuwahamasisha viongozi wa dini kuhusu mfuko huo ili wasaidie kuwahamasisha wananchi ambao wengi ni waumini wa misikitini na makanisa.
Akifungua kikao hicho, Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela amesema ana imani kubwa na viongozi wa dini katika kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya Afya kwa sababu viongozi wa dini wamekuwa msaada kwa Serikali katika masuala mbalimbali ya kijamii kwa kuwaelewesha wananchi.
“Ni imani yangu kuwa, kila mwananchi ana namna yake ya kuweza kuabudu, viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kuwafikia wananchi pamoja na kuwa Serikali inafanya pia”. Amesema Msovela.
Msovela amewaeleza viongozi hao wa dini kuwa CHF iliyoboreshwa inafanya kazi katika Mikoa mitatu kwa sasa ambapo Shinyanga ni mojawapo ya Mikoa hiyo, hivyo amesema ni bahati kubwa kwa wananchi wa Mkoa kutumia nafasi hii ili kupata matibabu kwa unafuu kwani kwa shilingi elfu kumi tu kwa mwaka, kaya yenye watu 6 watapata matibabu.
Awali, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Rashid Mfaume akimkaribisha Katibu Tawala Mkoa kufungua kikao hicho amesema, lengo la kikao ni kuwaomba Viongozi wa dini kusaidia kuwahamasisha waumini kujiunga na mfuko wa bima ya jamii iliyoboreshwa, kuhakikisha kuwa, jamii tunayoisimamia inapata huduma. “Jamii yetu wananchi wengi wana kipato kidogo, Serikali imeona kuwa kuna umuhimu mkubwa wa wananchi kupata huduma kwa gharama wanayoimudu”.
Dkt. Mfaume amesema, kutokana na kasi ya uandikishaji kuwa ndogo, Mkoa umewashirikisha viongozi wa dini ambao wataongeza kasi ya uhamasishaji na kusaidia waumini kuona namna ya kuwasaidia wananchi wasio na uwezo kuweza kupata huduma za afya kupitia CHF, hivyo ni vema waandikishaji hawa wafahamike na kuweza kuandikisha wanachama wengi zaidi.
Katika kikao hicho, Mkoa na viongozi hao wa dini wamekubalian masuala mbalimbali ikiwemo kufanya utaratibu wa kupata waandikishaji watakaoandikisha katika nyumba za Ibada, waratibu wa CHF wa Wilaya wafanye utambuzi wa viongozi wa dini katika maeneo yao ili wakae pamoja kupanga mkakati wa uhamasishaji.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa