Wadau watoe elimu kuwazuia vijana kufanya ngono, siyo matumizi ya kondomu
Wadau wa masuala ya afya na uzazi wamesisitizwa kutoa elimu zaidi ya kuwataka vijana kuepuka kufanya ngono katika umri mdogo, badala ya kuwasisitiza kutumia kondomu na njia nyingine za uzazi wa mpango.
Akizungumza na washiriki wa warsha ya kufunga mradi wa “DREAMS’ uliotekelezwa kwa miaka miwili na shirika la “amref health Africa” katika Mkoa wa Shinyanga, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amesema ni vema wadau wawe pamoja na Serikali katika kuwajengea uzalendo watoto.
“Suala la kutumia vizuizi si salama sana, watoto wadogo waachane na ngono utotoni wanakimbilia wapi? Hebu tujikite kwanza kuwataka hawa watoto waache ngono utotoni. tunapotoa njia hizi tukaona wanazikimbilia tunakuwa tunafungua milango ya zinaa, muda wao bado” Amesema Telack.
Amesisitiza kuwa vijana wenye umri wa miaka 15 – 16 bado ni wadogo sana.
Amewataka pia Watumishi wa vituo vya Afya pia wakiona watoto hao wanakwenda kutafuta kinga wawaulize ili wanaume wanaowarubuni wakamatwe kwani hata dini zinakataza kujiingiza kwenye ngono katika umri mdogo.
Amesema wengine wakipata njia hizi wanaenda kufanya ngono zembe, matokeo yake hatuwezi kupunguza maambukizi ya VVU. Walimu waseme na watoto wa kike waache kujiingiza kwenye vishawishi.
Hata hivyo amewapongeza shirika la “amref” waliofanya kazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Wilayani Kahama kwa kuchangia pia kupanda kwa ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne mwaka jana ambapo Mkoa umeshika nafasi ya tatu kutoka nafasi ya nne mwaka 2017.
Aidha, Mhe. Telack ametumia pia nafasi hiyo kuwaomba waone sababu ya wao kubaki kufanya kazi Mkoani hapa na kupanua wigo katika Halmashauri nyingine.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa