Wafanyabiashara wa Mkoa wa Shinyanga na Mikoa jirani wametakiwa kujipanga na kuchangamkia fursa za uwekezaji katika mradi wa bomba la mafuta ghafi Afrika Mashariki hususani kwenye maeneo yatakayopitiwa na bomba hilo linalojengwa kutokea nchini Uganda hadi Mkoani Tanga.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na wadau zaidi ya 100 walioshiriki warsha ya kujadili fursa za ushiriki wa Watanzania katika mradi huo, iliyofanyika mwanzoni mwa wiki hii Mkoani Shinyanga, amesema bomba hilo litapita ndani ya Mikoa 10 ya Kagera, Mwanza, Geita, Shinyanga, Mara, Tabora, Singida, Manyara, Arusha, Tanga na Simiyu na litawanufaishwa Watanzania wote hasa wa Mikoa hii.
Mhe. Mhagama amesema Serikali inatekeleza Sera na miongozo iliyowekwa kwa lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi hivyo bomba hili ni moja ya miradi ya kimkakati kati ya miradi mikubwa Nchini na utatumia tekinolojia mpya katika sekta ya mafuta.
Mhagama amesema kuwa, warsha hiyo ya siku mbili ambayo itafanyika pia katika Mikoa hiyo 10 itawasaidia wadau kujifunza fursa zitakazojitokeza wakati mradi huu utakapoanza kujengwa hadi kukamilika kwake na ndiyo sababu Baraza la uwezeshaji wananchi kiuchumi limeamua kupita kwenye Mikoa hii.
Amewataka wataalamu kufanya utafiti na kuhakikisha kuwa, Watanzania wote wanapata habari sahihi kuhusu fursa zitakazopatikana ili ziweze kufanyiwa kazi katika ubora na viwango vinavyotakiwa.
"Tumekubaliana kuwa, kupitia dira ya Taifa na mipango mbalimbali ya maendeleo kufikia mwaka 2025, sasa ni wakati wa Watanzania kuamka na kuyafahamu mambo mazuri yanayofanywa na taifa lao, miradi mikubwa inayotekelezwa na kwa kiasi gani ina uwezo wa kuwashirikisha waz kutumia fursa ya kuwaendeleza kiuchumi" amesema Mhagama
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewahimiza Wafanyabiashara kujipanga sasa kuwekeza kwenye Mkoa kwani mradi huu utakuwa na fursa nyingi sana, "tuhakikishe fursa zinazokuja kwenye bomba la mafuta zisiwe changamoto kwenu, mjipange kuhakikisha mnainuka kiuchumi"
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa