Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewataka wafungwa walioachiwa gerezani kwa msamaha wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli kubadilika na kuacha uhalifu watakapokuwa uraiani.
Akizungumza na baadhi ya wafungwa hao kati ya wafungwa 74 walioachiwa kwa Mkoa mzima mapema leo tarehe 10/12/2019 katika Gereza la Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Telack amewaasa kutorudia makosa yaliyowapeleka gerezani vinginevyo wakirudi tena hawatapata msamaha huo.
"Anachoamini Rais ni kuwa mmejutia makosa mliyoyafanya, ni matarajio yetu leo mmetoka mnaungana na familia zenu, muache kufanya uhalifu" amesema Telack.
Amewasisitiza kwenda kufanya kazi zinazowawezesha kuishi ikiwemo kilimo hasa wakati huu wa mvua pamoja na kuwa na hofu ya Mungu.
Nao baadhi ya wafungwa waliopata msamaha wa Rais wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli na kuahidi kuwa raia wema wanaporudi uraiani.
Akitoa taarifa ya wafungwa walioachiwa, Afisa Magereza wa Mkoa Kamishna Msaidizi Wilson Rugamba amesema kuwa katika magereza yaliyopo Mkoani ya Shinyanga ambayo ni gereza la Shinyanga na Gereza la Wilaya ya Kahama, walioachiwa kwa msamaha wa Rais ni wafungwa 74.
Mhe. Rais Magufuli ametoa msamaha huo kwa zaidi ya wafungwa 5000 hapo jana tarehe 09/12/2019 wakati akitoa hotuba ya maadhimisho ya siku ya Uhuru ambayo ni idadi kubwa ya wafungwa kupata msamaha huo.
Baadhi ya Wafungwa wa Gereza la Shinyanga walioachiwa kwa msamaha wa Rais
"Rais anaamini mmejutia makosa yenu badilikeni fanyeni kazi, huko nje zipo kazi nyingi za kuwawezesha kuishi ikiwemo kilimo" Mhe. Telack
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa