Waganga Wakuu wa Mikoa yote wameagizwa kuhakikisha kila Hopitali inakuwa na dawa maalumu kwa ajili ya wazee pamoja na kuwabaini Wazee wote ili wapate huduma za afya bila malipo.
Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Hamis Kigwangala ametoa agizo hilo alipotembelea kituo cha Wazee kilichopo katika Manispaa ya Shinyanga Mkoani hapa hivi karibuni.
" Hakuna maana yoyote kama mzee anapimwa na tatizo lake linafahamika halafu akifika kwenye dirisha la dawa anaambiwa dawa zimeisha kanunue" amesema Kigwangala.
Mhe. Kigwangala amewahakikishia Wazee kuwa, Serikali itahakikisha hali ya upatikanaji wa huduma za jamii, chakula, malazi na dawa inaimarika ikiwemo mikakati madhubuti ya kuwapatia huduma bila malipo na kuwalinda.
Amesema kulingana na sensa ya mwaka 2013 idadi ya Wazee nchini ni milioni 2.5 ambayo ni sawa na asilimia 5.6 ya wananchi wote na inakadiriwa kuongezeka na kufikia wazee 2.7 mwezi Desemba, 2017, hivyo Wizara inasimamia maslahi na kuhakikisha wanapata haki zao za msingi.
Awali, Mwenyekiti wa kituo cha Wazee Kolandoto Mzee Somola Maganga na Katibu wa Wazee Mkoa wa Shinyanga Mzee Sengerema wameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa jitihada kubwa ya kuwajali wazee na kutekeleza yale waliyoomba.
Aidha, Wazee hao wameomba kuwa na Daktari bingwa wa magonjwa ya wazee hususani ugonjwa wa tezi dume ambapo Waziri amewahakikishia kuwa, hospitali lazima ziwe na dawa maalumu kwa ajili ya wazee pamoja na kuwepo madaktari.
Kuhusu watumishi wa Idara ya ustawi wa jamii, Mhe. Kigwangala amesema Wizara itaendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili ili waweze kutekeleza majukumu yao vema.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri ameweka jiwe la msingi ujenzi wa bweni la wazee wa kituo cha Kolandoto litakalobeba wazee 20, amefungua jiko la gesi, amekabidhi bajaji pamoja na kiboksi cha huduma ya kwanza kwa wazee hao.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa