Na. Paul Kasembo, SHY RS
AFISA Serikali za Mitaa Mkuu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Fabian Kamoga amewataka Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga kujaza taarifa sahihi za utekelezaji wa shughuli za maeneo mnayosimamia ili kuepusha kuwepo kwa utata pindi wanapowasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye Kata zao na vikao vyao.
Kamoga ameyasema haya leo tarehe 31 Oktoba, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambapo pia amewataka Waheshimiwa Madiwani kufanya vikao kwa ukawaida ili kuhakiki taarifa wanazopokea kutoka kwa watendaji wa kata na kuona namna wananchi wanavyoshirikishwa katika shughuli za kuleta maendeleo katika kata husika.
“Waheshimiwa Madiwani niwaombe mtumie vizuri wakati wenu kuhakikisha kwamba mnajaza taarifa sahihi za maeneo mnayosimamia ili kuepusha kutokea kwa utata pindi mnapowasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika vikao vya Baraza kama hivi lakini pia hakikisheni mnafanya vikao kwa ukawaida ili mpate fursa ya kuhakiki taarifa mnazopokea kutoka kwa watendaji wa kata zenu,” amesema Kamoga.
Akishuhudia mawasilisho ya Waheshimiwa Madiwani kuhusu taarifa za utekelezaji miradi, Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Mwl. Alexius Kagunze amekiri kupokea taarifa zote zilizojadiliwa kwenye vikao na kuahidi kushirikiana na viongozi husika kuhakikisha yanaenda kufanyiwa kazi kwa ufanisi zaidi yote yaliyoainishwa.
Hiki ni Kikao cha Baraza la Madiwani robo ya kwanza 2024/2025 ambacho kimelenga kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye kata za Manispaa ya Shinyanga ili kuona ushirikishwaji wa wananchi kwenye kuleta maendeleo katika kila kata zetu.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa