Wadau wa Ushirika Mkoa wa Shinyanga wamewataka wakulima kutambua kuwa umiliki wa vyama vya ushirika ni wa wakulima wenyewe na siyo Serikali.
Wakijadili katika kikao cha pamoja cha wadau wa ushirika Mkoa, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wadau hao wamesema changamoto kubwa inayoua vyama vya ushirika ni wanachama wa vyama hivyo kutotambua umiliki wao.
Wamesema ifike mahali wanachama wajue kuwa ushirika una wenyewe.
Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika cha KACU Bw. Emmanuel Charahani amesema changamoto kubwa ni kutobadilika kwa uongozi kwenye vyama vingi vya ushirika kwa muda mrefu hivyo wenyeviti na mameneja hao kuwa kama watemi kwenye maeneo husika na matokeo yake wanachama wanashindwa kutambua umiliki wao.
Awali, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na uzalishaji Bw. Dotto Maligisa alisema kuwa vyama vya ushirika ni moja ya vikundi vinavyowezesha wananchi kiuchumi ndiyo sababu ya kujadili ili kuinua uchumi wa nchi.
Akitolea mfano wa zao la pamba, Bw. Maligisa amesema nchi nyingi Duniani zimekuza uchumi kutokana na viwanda vya nguo ambapo asilimia kubwa ya nguo tunazovaa zinatokana na zao hilo hivyo, Mkoa wa Shinyanga kwa kuwa ni kati ya Mikoa inaongoza kwa kilimo cha Pamba una dhamana kubwa ya kuhakikisha unainua zao hili kupitia Wakulima ambao ndiyo wanachama wa ushirika.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na Kaimu mrajis wa vyama vya ushirika Mkoa wa Shinyanga Bibi Shose Monyo, maazimio mbalimbali yamewekwa yenye lengo la kuinua ushirikia, ikiwemo kuhakikisha usimamizi kwa wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vya msingi na vyama vya ushirika waweze kujitambua na kumiliki vyama hivyo.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa