Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita ametoa agizo kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri mkoani humo kuhakikisha wanasimamia kikamilifu hali ya usafi wa mazingira kuanzia ngazi ya Kitongoji/Mtaa, Kijiji hadi Kata, kama sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya Afya ya Jamii na Mazingira Salama.
Akizungumza leo Septemba 16, 2025, wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Mikataba ya Lishe kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Mhita amesema kuwa suala la usafi ni ajenda ya kudumu inayohitaji uwajibikaji wa pamoja na ufuatiliaji wa karibu kutoka kwa viongozi wa ngazi zote.
“Kila Jumamosi iwe ni siku ya usafi wa mazingira katika maeneo yote ya Halmashauri, na Jumamosi ya mwisho wa mwezi ifanyike usafi mkubwa unaojumuisha mitaro, masoko, maeneo ya wazi na taasisi.” amesisitiza Mhe. Mhita.
Mkuu wa Mkoa pia ametumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa utekelezaji wa Mkataba wa Lishe, akiwataka watendaji kuhakikisha Siku za Afya na Lishe za Vijiji zinafanyika ipasavyo, zenye lengo la kutoa elimu ya lishe, kupima hali za watoto na kutoa rufaa za haraka kwa wanaohitaji msaada wa kiafya.
Vilevile, alielekeza kuwa kila shule ya msingi na sekondari kuhakikisha watoto wanapata chakula cha mchana shuleni, jambo ambalo linachochea afya bora, ufanisi wa ujifunzaji na mahudhurio ya wanafunzi.
“Shule zisizo na mpango wa chakula ni lazima zianzishe haraka, hili ni suala la kipaumbele. Hatutaki kuona mtoto anasoma akiwa na njaa, ni jukumu letu kuhakikisha hilo linatimia,” alisisitiza.
Mhe. Mhita alihitimisha kwa kusema kuwa maendeleo ya sekta ya afya na elimu hayawezi kutenganishwa na usafi wa mazingira na lishe bora. Hivyo, viongozi wote wanapaswa kuona kuwa ni wajibu wao kuhimiza, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo hayo kwa vitendo.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa