Wamiliki wa Vituo vya Kulelea Watoto Mchana (Day Care Centres) katika Manispaa ya Shinyanga wamehamasishwa kuvisajili vituo vyao kwa mujibu wa sheria na taratibu ili kuhakikisha watoto wanaolelewa katika vituo hivyo wanakuwa katika mazingira salama, rafiki na yanayozingatia haki za mtoto.
Wito huo umetolewa na Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Bi. Sarah Sanga, wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha wamiliki wa vituo hivyo, kilichofanyika jijini Shinyanga.
Bi. Sanga amesisitiza kuwa ni muhimu kwa kila mmiliki kuhakikisha kituo chake kimesajiliwa rasmi na kina cheti halali kilichosainiwa na Kamishna wa Ustawi wa Jamii, kama uthibitisho wa kutambuliwa na Serikali.
“Ninawasihi na kuwahamasisha wamiliki wote wa vituo vya kulelea watoto mchana kuvisajili vituo vyao ili vitambuliwe rasmi. Lengo letu ni kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama na yenye staha. Usajili huu ni kinga kwa watoto, kwa wamiliki na kwa jamii,” alisema Bi. Sanga.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga, Bi. Lydia Kwesigabo, alisema kuwa kikao hicho ni sehemu ya maandalizi ya Wiki ya Ustawi wa Jamii inayotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 25 hadi 30, 2025, ambapo pamoja na elimu, huduma za usajili wa vituo zitatolewa.
Aliongeza kuwa usajili huo utasaidia kuimarisha huduma zinazotolewa na vituo hivyo, pamoja na kujenga mtandao rasmi wa umoja wa wamiliki wa vituo katika mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na uboreshaji wa huduma.
Akizungumza kwa niaba ya wamiliki wa vituo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Vituo vya Kulelea Watoto Mchana, Bi. Damari Morris, aliwahimiza wamiliki wote ambao hawajasajili vituo vyao kutumia fursa ya Wiki ya Ustawi wa Jamii kujitokeza kwa ajili ya kusajili na kurasimisha huduma zao.
Kwa ujumla, kikao hicho kilitambua mchango wa vituo vya kulelea watoto mchana katika ukuaji wa mtoto, huku kikisisitiza umuhimu wa kufuata miongozo ya serikali ili kuwalinda watoto dhidi ya mazingira hatarishi.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa