Mashindano ya michezo kwa shule za sekondari (UMISSETA) Mkoani Shinyanga, yamefunguliwa rasmi kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya kitaifa ya UMISSETA yatakayofanyika Mkoani Mwanza.
Akifungua mashindano hayo yaliyofanyika katika shule ya sekondari Don Bosco Didia Wilayani Shinyanga, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewataka wanafunzi kutumia vizuri viwanja vya michezo kuonesha vipaji na uwezo wao ili ipatikane timu itakayowakilisha vizuri kitaifa.
Mkuu wa Mkoa amewaeleza wanamichezo hao kuwa michezo ni ajira, afya na furaha hivyo wasiache hata kwa ambao hawatapata nafasi ya kuwakilisha kitaifa. Telack amewaambia kuwa wakijituma watapata ajira kupitia michezo itakayowapeleka kitaifa na kimataifa akitolea mfano wachezaji wanaoiwakilisha Tanzania katika michezo mbalimbali kimataifa.
Mhe. Telack amesema, Serikali itahakikisha wanafunzi hao wanaofikia 598 na walimu 54 wanakaa vizuri kambini hapo ili wafanye vizuri katika maandalizi hayo.
Telack pia ameishukuru kampuni ya vinywaji baridi ya Coca Cola kwa kudhamini mashindano hayo, ambapo amepokea vifaa mbalimbali vya michezo ikiwemo jezi na mipira itakayopelekwa kwenye shule zote za Sekondari Mkoani hapa.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Mkoa Bw. Albert Msovela amemshukuru Mhe. Telack kwa kuyapa uzito na umuhimu mkubwa mashindano hayo ambapo timu ya Mkoa itakayopatikana itaenda kushindana Kitaifa.
Msovela amesema anaamini vijana hayo wameandaliwa na watajiandaa vizuri na wana ari kubwa hivyo ni hazina kubwa ya Taifa ambayo baadaye itakuwa ni wawakilishi wazuri hata Kimataifa.
Amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa, itakuwa ni fursa nzuri kwa wanafunzi hawa baada ya mashindano wataweza kushiriki na kuutangaza Mkoa katika nyanja mbalimbali kupitia ushiriki na ushindani wao. Hivyo walimu wahakikishe wanapata timu nzuri itakayowakilisha vema.
Aidha, Msovela ametumia nafasi hiyo kuzipongeza timu mbili za Stand United na Mwadui kwa kufanya vizuri katika mashindano ya ligi kuu ya Tanzania hivyo kuutangaza Mkoa wa Shinyanga katika tasnia ya Michezo, hivyo anaamini vijana hao wanafunzi watatengeneza pia nafasi kwa siku za baadaye baada ya kumaliza masomo yao.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa