Wananchi wa Kahama wamshukuru Rais Magufuli kwa kuwachangia ujenzi wa shule
Shule ya msingi Mayila iliyopo Mtaa wa Mayila, kata ya Nyihogo Wilaya ya Kahama imefunguliwa rasmi huku wananchi wa kata hiyo wakimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kwa kuwachangia shilingi mil. 5 ili kuhakikisha shule hiyo inakamilika.
Wazazi hao wametoa shukrani hizo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack alipokwenda kukagua utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais la kuhakikisha shule hiyo inafunguliwa mapema jana tarehe 07 Januari, 2020.
Wamesema kuwa, kukamilika kwa shule hiyo kutawapunguzia adha ya umbali wa zaidi ya kilomita 3 watoto wa kata hiyo waliokuwa wanalazimika kuvuka barabara kubwa kufuata shule kata za jirani hali iliyopelekea kuwa katika hatari ya kugongwa na magari.
“Nashukuru sana kwa shule hii, watoto wetu mwanzo walikuwa wanakwenda mbali na sisi kama wazazi tupo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali kujenga maboma” amesema Bw. Richard Joseph.
Diwani wa kata ya Nyihogo Mhe. Shadrack Mguami amesema, “kuna wakati naamka usiku kumuombea Mhe. Rais, sikutegemea kupata fedha kutoka kwake kwani angeweza kufanya shughuli nyingine lakini akaona atoe hapa, tunaahidi tutaendelea kumuunga mkono kwa kujenga maboma”
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kahama Mji Bw. Anderson Msumba amesema watoto zaidi ya 200 wameandikishwa kuanza darasa la kwanza hivyo uhitaji ni mkubwa, hata hivyo Halmashauri inaendelea kukamilisha maboma 108 na kufunga shule mpya 8.
“Tunamshukuru Mhe. Rais ametupa mori kuhakikisha shule hii inafunguliwa” amesema Msumba.
Mhe. Rais alichangia shilingi milioni 5 ili kuongeza nguvu ya kukamilisha shule hiyo alipopita Wilayani Kahama akielekea Wilayani Chato mwezi Novemba, mwaka jana 2019 na kuagiza ifunguliwe mwezi Januari mwaka huu 2020.
Shule hiyo iliyokuwa na vyumba viwili vya madarasa, hivi sasa ina vyumba 8 na matundu ya vyoo 12.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa