Na. Shinyanga RS.
Wananchi wa Kijiji cha Ugela wameonesha shangwe kubwa kwa MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Solomon Mndeme ambaye amekuwa RC wa kwanza kufika tangu kuanzishwa kwa kijiji hicho kilichopo Kata ya Ulowa Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama huku akiwaeleza namna ambavyo Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyowajali na hata sasa inaboresha na kuwasogezea huduma karibu yao.
Hayo yametokea leo tarehe 18 Septemba, 2023 ambapo Mhe. Mndeme akiwa katika utaratibu wake wa ziara za kutembelea, kuongea, kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Halmashauri zote za Mkoa wa Shinyanga ambapo kwa Wilaya ya Kahama ameongozana na Mkuu wa Wilaya Mhe. Mboni Mhita @mboni_mhita, Kamati za Usalama, Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe. Emmanuel Cherehani, wataalam mbalimbali kutoka Taasisi kama Wakala wa Umeme Vijijini (REA), RUWASA na TARURA kwa lengo la kutatua kero zao.
"Ndugu zangu wananchi wa Kijiji hiki cha Ugela, asanteni sana kwa mapokezi yenu makubwa, napokea pongezi za kuwa Mkuu wa Mkoa wa kwanza kufika hapa tangu kuanzishwa kwa kijiji hiki. Pamoja na hayo naomba niwaambia kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawajali sana kama mnavyoona imeleta fedha nyingi sana katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, nishati ya umeme, miundombinu nk," alisema Mhe. Mndeme.
Katika mkutano huo wa hadhara kero mbalimbali zilitajwa na kupatiwa ufumbuzi ikiwemo kukosekana kwa usalama, mawasiliano ya simu, maji, barabara na upungufu wa watumishi sekta ya afya.
Akijibu kero hizo Mhe. Mndeme aliaguza uongozi wa Polisi Mkoa kuhakikisha Kituo Kidogo cha Polisi kinakamalika haraka na kuletwa askari katika eneo hilo kwakuwa kituo kilikwisha anza kujengwa tayari. Aidha kuhusu mawasiliano tayari Kampuni ya Vodacom wamekwishafika na kusaini katika Serikali ya Kijiji na sasa wapo mbioni kuanza ujenzi wa mnara.
Kero ya maji ilitolewa ufafanuzi kuwa mradi wa maji ya Ziwa Victoria unakuja na moja eneo litakolonufaika ni Kijiji cha Ugela.
MATUKIO KATIKA PICHA
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa