Serikali imewatangazia wananchi wa kata ya Maganzo, Wilaya ya Kishapu kuanza kuchenjua mchanga unaotokana na madini ya Almasi ndani ya mwezi huu.
Waziri wa madini mhe. Dotto Biteko amewatangazia neema hiyo wakati wa mkutano na wananchi hao uliofanyika Maganzo hapo jana tarehe 10/12/2019 na kusema kuwa kuanzia tarehe 22 Desemba Mgodi wa Mwadui utaanza kutoa mchanga huo nje ya mgodi.
"Miaka yote mlikuwa mnalilia mchanga, mchenjue tumekubaliana na mgodi nimeshawaambia tar 22 mwezi huu mchanga utatolewa kule ndani, nipate taarifa tarehe hiyo kuwa mchanga umeanza kutoka" amesisitiza Biteko.
Mhe. Biteko amewataka wananchi wa Maganzo kuhakikisha wanapopata Almasi wapeleke kwenye soko wauze ili walipe kodi, isiwe ni uchochoro wa kuitorosha.
Biteko pia amemuagiza Afisa Madini Mkoa kuhakikisha kuaniza Januari mwaka 2020, asilimia 5 ya Almasi inabaki kuuzwa kwenye soko la Maganzo ili kuinua uchumi wa wananchi.
Amesema mhe. Rais Magufulu ameitoa mbali sekta hii tangu Almasi ilikuwa inachukuliwa kupelekwa Ulaya wakati Wanamaganzo wamebaki masikini. "Mhe. Rais anachotaka ni Almasi na madini mengine nchini yabadilishe maisha ya wananchi, kwenye hili Rais hana mchezo " amesisitiza Biteko.
Amesema hivi sasa katika sekta ya madini mapato yamepanda hadi sh. bil 470 kutoka sh. bil 190 kutokana na kuanzisha mfumo wa masoko ili kodi ibaki Tanzania itumike kujenga madarasa, kuongeza miundombinu na madawa hospitalini.
Wananchi wa Maganzo, Kishapu watangaziwa neema ya kutumia mchanga wa Almasi
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa