Waziri wa Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni Mhe. Harrison Mwakyembe amewakumbusha Wananchi kushiriki na kudumisha amani katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 24 Novemba, 2019.
Akizungumza katika Misa ya Jubilee ya miaka 25 ya upadri wa Askofu Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, iliyofanyika mapema leo tarehe 14 Novemba, 2019 kwenye Parokia ya Mama mwenye huruma Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Mwakyembe amewahimiza Watanzania kujitokeza kupiga kura kwa amani na kumuweka Mungu mbele.
Mhe. Mwakyembe ambaye amekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ya Jubilee kwa niaba ya Mhe. Samia Suluhu, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema, Serikali ya awamu ya tano inaamini kuwa bila Mungu hakuna mafanikio yoyote yanayoweza kuendelea, hivyo ametumia nafasi hiyo kuwaomba Viongozi wa dini kuendelea na kazi kubwa wanayoifanya kila siku ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
"Tunaweza kujenga majengo, kununua ndege za kila aina, kuwa na ulinzi wa majeshi yote lakini bila baraka za Mungu hakuna maana, ndiyo maana Rais kila mara anasikika akisema naomba mniombee" amesema Mhe. Mwakyembe.
Katika maadhimisho hayo ya Jubilee ya miaka 25 ya upadri wa Askofu Sangu, Viongozi mbalimbali wa Serikali wamehudhuria pia akiwemo Mama Anna Makinda, Spika wa Bunge Mstaafu, Mhe. Nape Nnauye, Mbunge wa Jimbo la Mtama pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Patrobas Katambi.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa