Wananchi wametakiwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi kulinda mipaka ya Kambi na kukaa mbali ili kujiepusha na madhara yanayoweza kutokea kwa sababu ya mazoezi mbalimbali ya Jeshi yenye lengo la kulinda usalama wa Raia.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack ameyasema hayo jana tarehe 03/12/2019 katika Mkutano na wananchi wa Kijiji cha Mwamashele, Kata ya Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga ambapo wananchi hao walidai wamezuiliwa kufanya shughuli za kilimo kwenye eneo la Jeshi.
Mhe. Telack amesema ni agizo la Serikali maeneo yote ya Jeshi nchi nzima kuwekwa mipaka hivyo wananchi hao waendelee kulima maeneo mengine waliache eneo la Jeshi ili wasije kupata madhara iwapo yatatokea kutokana mazoezi ya Jeshi.
Amesema ana taarifa zote kuwa wananchi walikuwa wanalima eneo hilo la Kizumbi na kama Serikali inafurahishwa na jambo hilo kwa sababu wanazalisha lakini kwa usalama wao na Taifa kwa ujumla ni vema kukaa mbali kwani kutoka na changamoto za Kiusalama zinavyoongezeka na miundombinu ya usalama inaongezeka pia ikiwemo maeneo.
"Kambi zote zitawekwa mipaka kwa usalama wa wananchi, maeneo ya kulima yapo tusiingie eneo lililozuiliwa mtapata madhara hivyo tushirikiane kwa pamoja kama wananchi kulinda kambi yetu na tusiokote kitu chochote tusichokijua ili kujiepusha na matatizo" amesisitiza Mhe. Telack.
Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Manispaa ya Shinyanga Bw. Kenneth Chande ametumia nafasi hiyo pia kuwafafanulia wananchi hao sheria ya ardhi kuhusu fidia ambapo walidai wananchi wengine walilipwa lakini wenyewe hawakulipwa na kuwaeleza kuwa, wananchi waliolipwa kipindi hicho ardhi inatwaliwa na Jeshi, walilipwa fidia ya eneo lililokuwa limeendelezwa wakati huo.
Naye Kiongozi wa Jeshini hapo amesema eneo hili lilitengwa kwa ajili ya mafunzo ya Jeshi hivyo amewaomba wananchi kuacha kufanya shughuli ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa