Wananchi wa Manispaa ya Shinyanga ambao wameuziwa kiwanja kimoja zaidi ya mtu mmoja wametakiwa kupeleka taarifa zao kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga kwa lengo la kupewa viwanja vingine.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Bw. Geoffrey Mwangulumbi amesema jana katika mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga uliokuwa na lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.
Bw. Mwangulumbi amesema kuwa, taarifa zikishahakikiwa na kubaini wananchi waliogongana kwenye kiwanja kimoja, wananchi hao watapewa viwanja vingine bure.
Amesema Manispaa ina mpango wa kuwapa viwanja wananchi hao ili kumaliza migogoro hiyo ya “double allocation” ambayo ni mingi na kufika mwezi Septemba mwaka huu watakuwa wameanza mpango huo.
Aidha, akifunga mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewataka Maafisa Ardhi kuanza kutoa elimu ya umiliki wa viwanja na kila mwananchi atakayepimiwa aoneshwe eneo lake.
Katika mkutano huo, wananchi wameweza kutoa kero mbalimbali ambapo kero za ardhi zimeonekana kuongoza hali iliyomlazimu Mkuu wa Mkoa kumtaka Mkurugenzi wa Manispaa pamoja na wataalamu wa ardhi kuhamia maeneo yenye kero kubwa ili kuzimaliza kabisa.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa