Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewataka Wanaume wote mkoani Shinyanga kuwekeza zaidi kwenye afya zao kwani wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanaleta mabadiliko chanya katika familia, jamii na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema haya leo tarehe 19 Novemba, 2024 kwenye maadhimisho ya siku ya wanaume Duniani ambayo kwa Mkoa wa Shinyanga yamefanyika kwenye Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM) huku akisisitiza kuwa anatambua wanaume wana harakati za kutafuta na kukuza uchumi, lakini kuna wakati utafika yeye mwanaume na mali yake yote aliyoichuma kwa muda mrefu wote kwa pamoja watalazimika kuipambania afya.
“Ninawataka wanaume wote ambao mmehudhuria kwenye maadhimisho haya na wengine pia ambao hawakupata nafasi ya kushiriki nasi, mjitahidi kwa kiasi kikubwa na kuhakikisha mnafanya uwekezaji zaidi katika afya zenu kwenye harakati za kutafuta na kukuza uchumi kwani msipofanya hivyo kuna wakati utafika yeye mwanaume na mali yake yote aliyoichuma kwa muda mrefu wote kwa pamoja watalazimika kuipambania afya” amesema RC Macha
Maadhimisho ya siku ya wanaume Duniani yalianzishwa tarehe 19 Novemba, 1999 na Dkt. Jerome Teelucksingh ambayo yanalenga kuthamini matokeo chanya ya wanaume pamoja na kusherehekea maisha yao, mafanikio na michango wanayoitoa kwenye maendeleo katika nchi.
Katika maadhimisho haya ambayo pia yamehudhuriwa na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni. Pia yamejumuisha viongozi mbalimbali wa vyama, Serikali na wajumbe ambao ni wazee mkoani Shinyanga yana kauli mbiu inayosema “Mwanaume, kuwa mfano chanya katika jamii”.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa