Wanawake nchini wameaswa kuwa na tabia ya kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa Saratani za matiti na mlango wa kizazi ili kupata tiba mapema iwapo watagundulika kuwa na virusi vya Saratani hizo.
Wosia huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack wakati akizindua zoezi la utoaji chanjo mpya ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wa miaka 14 mapema leo katika eneo la Nguzo nane, Manispaa ya Shinyanga.
Katika hotuba yake ya uzinduzi Mhe. Telack amesema Saratani ya mlango wa kizazi ndiyo inayoongoza kusababisha vifo kwa wanawake kuliko saratani nyingine ndiyo sababu Serikali imeamua kutoa chanjo hii.
" Kwa mwaka, takribani wanawake 4000 wanafariki kwa sababu ya saratani hii" amesema Telack.
Aidha, amewataka wanawake kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya iwapo wataona dalili zozote za ugonjwa wa saratani.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Josephine Matiro amesema, Wilaya ya Shinyanga imetoa elimu kwa njia mbalimbali ikiwemo kupitia viongozi na watendaji wa ngazi zote ili wananchi wote waelewe umuhimu wa chanjo ya Saratani ya mlango wa kizazi na wote wananostahili kupata chanjo wafikiwe.
Awali, Katibu Tawala Msaidizi Afya katika Sekretarieti ya Mkoa Dkt. Rashid Mfaume amesema kuwa, uzinduzi wa chanjo ya saratani hii unafanyika nchi nzima ambapo wasichana wote wenye umri wa miaka 14 watapata chanjo hii.
Dkt. Rashid ameongeza kuwa, kuanzia mwaka ujao wasichana watakaopata chanjo hiyo ni wa miaka 9 - 14 na baadaye itakuwa inafanyika kila mwaka kwa wasichana wa miaka 9 lengo likiwa ni kuwazuia wasichana ambao hawajaanza kujihusisha na ngono kupata virusi vinavyosababisha Saratani hiyo.
Saratani za matiti na mlango wa Kizazi zinaelezwa kuongoza kuathiri wanawake hasa katika nchi zinazoendelea ambapo saratani ya mlango wa kizazi ndiyo inayoongoza kwa kusababisha vifo.
Wanawake 466,000 kila mwaka duniani wanagundulika kuwa na Saratani hii wakati nchini Tanzania wanawake 7304 wanaugua na kati ya hao 4,216 sawa na asilimia 58 hufariki.
Kwa Mkoa wa Shinyanga, wasichana walengwa wa kupata chanjo hiyo ni zaidi ya elfu 29.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa