Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia Elimu na Mafunzo ya Ufundi mkoani Shinyanga, Samson Hango, amesema jumla ya watahiniwa 41,463 wanatarajiwa kuanza mtihani wa kumaliza darasa la saba kuanzia kesho, Septemba 11, 2025 katika shule zote za msingi za Serikali na binafsi mkoani humo.
Akizungumza na Waandishi Wa Habari Ofisini kwake, Hango amesema kati ya watahiniwa hao, wasichana ni 23,938 na wavulana ni 17,525, huku akibainisha kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika ikiwa ni pamoja na usalama wa mitihani, mazingira ya shule, pamoja na maandalizi ya walimu wasimamizi.
Ameongeza kuwa jumla ya shule 664 zitashiriki katika mtihani huo, ambapo 598 ni shule za Serikali na 66 ni shule binafsi.
Aidha, Hango amesema kati ya watahiniwa wote, wanafunzi 54 wenye mahitaji maalumu watashiriki mtihani huo, wakiwemo wavulana 26 na wasichana 28, na tayari maandalizi ya kuhakikisha mazingira rafiki kwa kundi hilo yamefanyika.
Amewataka wazazi na walezi kuwahamasisha watoto wao kufanya mtihani kwa amani, utulivu na bila hofu, huku akiwasihi kuhakikisha watoto wao wanafika shuleni kwa wakati.
“Tunawatakia kila la heri watahiniwa wetu wote. Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri zote imejipanga kuhakikisha mitihani hii inafanyika kwa utulivu na uadilifu wa hali ya juu,” amesema Hango.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa