Watendaji wa Vyama Vikuu vya Ushirika (AMCOS) kutoka Mkoa wa Tabora wametakiwa kufanya kazi kwa ubunifu, maarifa na uadilifu ili kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya biashara kama tumbaku, pamba na mazao mchanganyiko kwa manufaa ya wakulima na uchumi wa mikoa yao.
Wito huo umetolewa Septemba 26, 2025 na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi – Utawala na Rasilimali Watu, Bw. David Lyamongi, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya vitendo kwa watendaji wa AMCOS, yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Ushirika (MoCU) Kampasi ya Shinyanga.
Lyamongi amesema mafunzo hayo ni nafasi ya kipekee kwa watendaji hao kujifunza namna bora ya kusimamia ushirika na kuwa chachu ya mabadiliko katika uzalishaji wa mazao ya biashara nchini.
“Mnapaswa kuwa wabunifu, msiwe wa kawaida. Ushirika wenu ndio dhamana ya wakulima, hivyo mnapaswa kuwapa maarifa, teknolojia na mbinu za kuongeza thamani ya mazao yao. Tutumie mafunzo haya kujijenga na kuleta matokeo chanya mashinani,” amesema Lyamongi.
Aidha, aliwataka viongozi hao kuendesha vyama vyao kwa uadilifu na ufanisi, wakizingatia Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013, huku wakiepuka ubadhirifu, uzembe na matumizi mabaya ya madaraka ili kudumisha imani ya wanachama na kuongeza mafanikio ya vyama vyao.
Kwa upande wake, Kaimu Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Tabora Jarufu Juma, amesema mafunzo hayo ya siku 14 yamelenga kuwajengea uwezo watendaji ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuleta matokeo chanya kwenye vyama vyao.
“Watendaji wetu wako tayari kujifunza na kutumia mafunzo haya kama chachu ya mabadiliko. Tunataka AMCOS zetu ziwe sehemu ya suluhisho la kiuchumi, si changamoto kwa wakulima,” amesema Jarufu.
Mafunzo hayo yanayoshirikisha zaidi ya washiriki 120, yanatarajiwa kuwa kichocheo cha mageuzi katika usimamizi wa AMCOS na kuinua uchumi wa wakulima kupitia ushirika imara, unaozingatia tija, ubunifu na uwajibikaji.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa