Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko amekataa tabia ya baadhi ya kampuni za Migodi kuwapa kipaumbele na kuwanyenyekea raia wa kigeni kuliko Watanzania.
Akizungumza na Wafanyakazi wa Mgodi wa Mwadui jana tarehe 10 Desemba, 2019 alipofanya ziara ya siku moja Mkoani Shinyanga, Mhe. Biteko amesema, kuna tabia katika baadhi ya Migodi, Watanzania wanakuwa wengi lakini maamuzi yanafanywa na watu wachache ambao mara nyingi ni raia wa kigeni hali inayosababisha wafanyakazi kukosa mahali pa kusemea changamoto zao.
Mhe. Biteko amesema Serikali ya Tanzania inataka kuona matatizo yanamalizwa bila uvunjifu wa sheria ikiwemo kuondoa manyanyaso mahali pa kazi na wafanyakazi kupata haki zao ili kuwapa motisha, kwani ndiyo wenye mchango mkubwa katika uzalishaji.
Akinukuu kifungu cha sheria ya madini ya mwaka 2017, pamoja na matakwa ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Magufuli, Mhe. Biteko amesema Watanzania wafanye kazi zozote zinaweza kufanywa na Watanzania zifanywe na Watanzania. Wageni wataajiriwa pale tu ambapo ujuzi alionao hauwezi kupatikana miongoni mwa Watanzania ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo Watanzania.
"Mgeni kuwa na mshahara mkubwa ni sawa kwa sababu ametoka mbali lakini si kweli kwamba awe na mshahara mkubwa mara tano zaidi ya wenyeji, hapana tunaanza utaratibu wa kuangalia 'payrol' za wafanyakazi wa migodini" amesema Biteko.
Amesisitiza kuwa kazi yake kubwa aliyopewa ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanafurahia maisha kwenye migodi bila kunyanyaswa na kuonewa na wageni wakipungua zaidi.
Hata hivyo, Biteko ameupongeza mgodi wa Almasi Mwadui kwa kuwa na mahusiano mazuri na wafanyakazi pamoja na uzalishaji mkubwa wa Almasi uliofikia karati laki 4 mwaka huu.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa