GEITA.
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa dini na Watanzania kwa ujumla wahakikishe wanasimamia na kuimarisha maadili mema kwa jamii ili kuepuka maovu na kuleta maendeleo endelevu kwa Watanzania.
“Nitumie fursa hii kuendelea kutoa rai kwa wananchi, wazazi na viongozi wa dini kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika malezi ya watoto wetu katika ngazi zote kwa kuzingatia maadili na tamaduni ya Taifa letu. Ni wajibu wetu kama wananchi”
Amesema hayo leo (Jumatatu, Septemba 16, 2024) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Baraza la Maulid Kitaifa lililofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyankumbu, Mkoani Geita.
Amesema kuwa viongozi wa dini wana jukumu la kutoa mwongozo na malezi ya kiroho kwa waumini kwa kuwa wana nguvu kubwa ya kuhamasisha maadili na tabia nzuri.
“Wazazi, ninyi mna jukumu la msingi katika kulea watoto wenu kuanzia katika ngazi ya familia ili kujenga tabia njema, na tukifanya hivyo matendo na hovyo hayatakuwepo, lazima tuwe macho katika matendo haya ambayo yanaweza kuleta hofu kwa jamii yetu”
Sambamba na msisitizo katika maadili, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kila mmoja ashiriki katika kulinda Taifa kwa kutambua matendo yote yanayoashiria uvunjifu wa amani ili nchi iendelee kuwa imara “suala la ulinzi na usalama ni letu sote watanzania, ndivyo tulivyofanya tangu Tanzania ipate uhuru”
Aidha amesema kwa kuenzi maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W), tutumie sherehe za Maulid kuwa chanzo cha mabadiliko chanya katika maisha ya waumini. Sote tutumie nafasi hii kuhamasika na kujitahidi kuishi kwa maadili ya Mtume, ambayo yanajumuisha tabia nzuri, uadilifu na huruma.
Kwa Upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Dkt. Abubakary Zubeir Ally amewataka waislam na Watanzania kushikiri katika ujenzi wa uchumi wa nchi ikiwemo ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika sekta za elimu na afya. “Waislam tujenge na tuulinde uchumi wetu, tusomeshe watoto ndani na nje ya nchi”
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa