Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amekamilisha ziara yake ya siku tano Mkoani Shinyanga leo tarehe 17 Julai, 2018.
Mhe. Majaliwa katika ziara yake, iliyoanza tarehe 13 Julai, 2018 ametembelea Halmashauri zote sita za Mkoa wa Shinyanga na kuzungumza na Watumishi wa Umma ambapo amewakumbusha wajibu wao katika kuwatumikia wananchi kwa kuwa waadilifu na waaminifu.
Katika Halmashauri zote Mhe. Majaliwa pia ameweza kukutana na wananchi ambapo amewaeleza mipango na kazi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano katika kuwaletea maendeleo pamoja na kuwaahidi kuzidi kuboresha utendaji, miundombinu ya maji, afya, elimu, umeme na barabara.
Baadhi ya shughuli alizozifanya ni pamoja na kuzindua mradi wa maji katika kijiji cha Isoso Wilaya ya Kishapu, kutembelea na kuona viwanda vya kuchambua pamba, kutengeneza mafuta katika Manispaa ya Shinyanga na kiwanda cha kuchambua mchele Halmashauri ya Mji Kahama, kuona ujenzi wa vituo vya Afya na kuzindua soko na ghala la wakulima katika kata ya Chela.
Aidha, Mhe. Majaliwa amezindua mpango wa kutoa Bima ya Afya kwa Wakulima kupitia vyama vya Ushirika ambapo Kitaifa uzinduzi umefanyika katika kijiji cha Kangeme, kata ya Ulowa, Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.
Mhe. Majaliwa ambaye aliambatana na Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias Kuandikwa pamoja na Naibu Waziri wa OR- TAMISEMI Mhe. Joseph Kakunda na viongozi wengine ametoa maagizo mbalimbali kwa viongozi na watendaji Mkoani hapa ikiwemo kuwafuata wananchi mahali walipo na kutatua kero zao badala ya kukaa Ofisini.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa