Na. Paul Kasembo, Shy RS.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Augustino Vuma (MB) imeiagiza Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Shinyanga kumsimamia Mkandarasi China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) anayetekeleza upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilishwa kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa ili kuleta tija ya miradi inayotekelezwa na Serikali.
Maagizo hayo yametolewa Machi 20, 2025 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Augustino Vuma baada ya kutembelea na kukagua Utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga mradi unaogharimu takribani Tzs. Bilioni 48 na ambao mpaka sasa umefikia asilimia 75% ya utekelezaji wake.
“Kamati inaiagiza Wizara ya Ujenzi na TANROADS mkoa wa Shinyanga kumsimamia Mkandarasi (CHICO) kwa ukaribu ili kuhakikisha kazi zote zilizobakia kwenye mradi huu zinakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia ubora ili kuleta tija kwenye miradi ambayo inatekelezwa na Serikali na hatimaye wananchi ambao ndio wanufaika wakubwa wafurahie matunda yake”, amesema Mhe. Augustino.
Aidha Kamati imeiagiza Wizara ya Ujenzi, TANROADS Mkoa wa Shinyanga pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kushirikiana kwa pamoja ili kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alipotembelea uwanja huu wa ndege na kuagiza uanze kutumika wakati wakisubiri jengo la abiria likamilike.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde, amekiri kupokea maelekezo na ushauri wa Kamati na kuahidi kuwa watafuata maelekezo yote ikiwa ni pamoja na kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi huu unakuwa wenye tija na unakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.
Akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Julius Mtatiro (Wakili) ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga ameishukuru kamati kwa kutoa maelekezo haya kwani huu uwanja utakapoanza kutumika utakuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi mkoani Shinyanga.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa