Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita @mboni_mhita ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara za ndani katika Manispaa ya Kahama na kuagiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya mkandarasi anayetekeleza mradi huo, Kampuni ya Sichuan Road and Bridge Group (SRBG).
Akiwa kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo unaotekelezwa kupitia Mradi wa TACTIC iliyofanyika Septemba 30,2025 RC Mhita amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Masoud Kibetu kuandika barua rasmi kwa mkandarasi huyo, ikiambatana na adhabu ya kukatwa milioni 2 kwa kila siku kuanzia Oktoba 1, 2025, baada ya mkataba wake kufikia ukomo tarehe 30 Septemba 2025, bila kazi kukamilika.
“Mkandarasi huyu amelipwa zaidi ya shilingi bilioni 5, lakini kasi ya utekelezaji ni ya kusuasua licha ya kuongezewa muda mara mbili. Serikali haina tena sababu ya kumuongezea mkataba,” alisema Mhita kwa msisitizo.
Amesema Serikali ya Mkoa haitavumilia kuona fedha za umma zinatumika bila matokeo halisi, akisisitiza kuwa kila mkandarasi anapaswa kuzingatia muda wa utekelezaji na thamani ya fedha inayotolewa kwa miradi ya maendeleo.
Katika maagizo yake, Mhita amesisitiza kuwa adhabu hiyo ya kisheria inalenga kulinda maslahi ya wananchi ambao wanasubiri huduma bora za miundombinu na kuonya kuwa hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa endapo mkandarasi atashindwa kumaliza kazi hiyo kwa haraka.
Ziara hiyo imekuwa sehemu ya msukumo wa kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo unakwenda kwa kasi inayostahili, huku RC Mhita akisisitiza uwajibikaji kwa watendaji wote na wadau wa ujenzi katika Mkoa wa Shinyanga
Nao baadhi ya wananchi waliokuwepo kwenye mradi huo walimpongeza RC Mhita kwa hatua alizochukua na kumuomba kumsimamia kwa ukaribu mkandarasi huyo katika kipindi ambacho Mvua zinatarajia kunyesha ili wasipate madhara yakiwemo mafuriko kutokana na kutokamilika kwa miundombinu katika manispaa ya Kahama.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita @mboni_mhita , ametembelea ujenzi wa barabara ya Mwawaza inayojengwa kwa kiwango cha lami na kutoa kauli madhubuti kuhusu umuhimu wa kukamilika kwa mradi huo kwa wakati.
Amesisitiza kuwa hatakubali kuona mtu au taasisi yoyote ikikwamisha ujenzi huo, kwani barabara hiyo ni mkombozi mkubwa kwa wananchi, hususan wagonjwa wanaosafiri kutibiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo na wakazi wanaopata shida ya kufikika kwa urahisi.
"Barabara hii ni uhai kwa watu wanaokwenda kutibiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ( Mwawaza) ni lazima ijengwe kwa viwango na kwa wakati.
Hakuna nafasi ya uzembe wala ucheleweshaji utakaokubalika kwenye ujenzi wa mradi huu," amesema RC Mhita kwa msisitizo.Ujenzi huo unatajwa kuleta mapinduzi katika sekta ya afya, biashara na usafiri kwa ujumla, na Serikali imejipanga kuhakikisha unakamilika kama ilivyopangwa.
Katika kuadhimisha Siku ya Usafishaji Duniani Septemba 20, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita ameongoza mamia ya wananchi kushiriki zoezi la usafi katika Soko la Kambarage, Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza na wananchi, Mhe. Mhita amesisitiza umuhimu wa kuzingatia usafi kama sehemu ya maisha ya kila siku na si tukio la mara moja.
Ameeleza kuwa soko hilo ni miongoni mwa maeneo yatakayofanyiwa maboresho kupitia mradi wa TACTIC, hivyo kuhitaji maandalizi bora ya mazingira.“Tuache kusubiri maagizo, tufanye usafi kwa kujitambua, kwa afya zetu, kwa heshima ya mji wetu,” amesema RC Mhita.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa CP Salum Hamduni amepongeza mwitikio wa wananchi na kutoa wito kwa jamii kuendeleza utamaduni huo kila siku.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa